DC ASIA ABDALLAH :IRINGA ACHENI MAJUNGU FANYENI KAZI KUKUZA KIPATO CHENU

 Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Asia Abdallah akizungumza na wanachama na wadau wa timu ya Lipuli kwenye mkutano wa uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya wa timu ya Lipuli uliofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Mwembetogwa.
Baadhi ya wadau na wanachama wa timu ya Lipuli wakiwa makini kumsikiliza mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Kilolo Bi Asia Abdallah

Na Fredy Mgunda, Iringa.

Mkuu wa wilaya ya kilolo Asia Abdallah aliwataka wananchi wa Mkoa wa Iringa kuishi bila kuwa na majungu kwa sababu majungu yanarudisha nyuma maendeleo.

Hayo aliyasema wakati wa hotuba ya uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya wa timu ya Lipuli katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Mwembetogwa  iliyopo Manispaa ya Iringa.

Abdallah alisema kuwa Iringa kumekuwa na majungu ambayo yamekuwa yakileta uchonganishi baina ya watu na watu pia viongozi na viongozi hivyo inatakiwa kubadilika na tusiishi kwa mazoea.

"Ukiingia huku majungu kule majungu hata mtu hana pesa ya kula lakini anashinda kwenye mitandao ya kijamii kuleta majungu, fanyeni kazi kwa nguvu zenu zote maana mnaendekeza tu majungu ambayo hayana manufaa kwako binafsi hata taifa kwa ujumla"alisema Abdallah

Aidha Abdallah alisema kuwa viongozi wa timu ya Lipuli watakaoingia madarakani wahakikishe wanavunja makundi yote ya majungu na kuhakikisha timu inakuwa na umoja na ushirikiano katika kila nyanja ili kupata mafanikio makubwa ambayo yataleta faraja kwa wakazi wa Iringa na wapenda Soka.

"Haiwezikani kila kona ni majungu tu hivi nyie hamna kazi za kufanya tena afadhali wanawake wangekuwa na majungu lakini majungu hayo yanaongozwa na wanaume kwenye magroup ya whatsup, achaneni na magroup ambayo hayana faida kwako wala hayana afya kwa taifa la Tanzania" alisema Abdallah

Bi Asia aliongeza kwa kusema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John pombe Magufuli, anahimiza wananchi kufanya kazi na sio kutengeneza majungu ambayo yamekuwa yakikwamisha maendeleo ya wananchi.

Kwa upande wake Katibu wa chama cha Soka Mkoani Iringa Dr Ally Ngalla alimshukuru Mkuu wa wilaya huyo kwa hotuba nzuri na kumuahidi kuwa Iringa itabadilika na kufuta majungu kutokana na tayari wamepata viongozi wapya wa timu ya Lipuli.

"Nikiwa kama kiongozi nitahakikisha makundi yote ya majungu yanavunjwa na kuwa kitu kimoja ambapo tutafanya kazi kama siafu ili kuinua mpira wa miguu Mkoani Iringa "alisema Ngalla

Ngalla aliwataka wadau wa mpira miguu mkoani Iringa kusahau yaliyopita na kuangalia nini cha kufanya ili kuisadia timu ya Lipuli ifanye vizuri kwenye ligi kuu Tanzania bara na kurejesha furaha ya wananchi wa Iringa.

Naye Mwenyekiti mpya wa timu ya Lipuli, Ramadhani Mahano aliwaomba wadau wa mpira na wapenzi wa timu ya Lipuli, kufanya kazi kwa ushirikiano pamoja kuvunja makundi yote yaliyokuwa yanasababisha migogoro ya Lipuli na mpira wa miguu kwa ujumla.

Nawaombeni sana kuyaweka kichwani vizuri maneno ya Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Bi Asia Abdallah, kwa kuacha majungu au kusababisha migogoro ambayo haina maana bali naomba tushauriane kwa kila jambo kwa manufaa ya Lipuli na wadau wa mpira.

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.