DC IRINGA APIGA MARUFUKU UVUVI SAMAKI WADOGO MTERA


Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela akizungumza katika moja ya vikao vya baraza la madiwani
MKUU wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amepiga marufuku wavuvi kuvua samaki wadogo katika bwawa la Mtera na kuwataka watendaji kuwachukulia hatua kali watakaokiuka agizo hilo. Hatua hiyo inatokana na wavuvi hao kukiuka agizo la kuvua samaki wadogo na kusababisha upungufu mkubwa wa samaki katika bwawa la Mtera kutokana na kushindwa kuendelea kuzaliana kwa kuua vizazi vya samaki.
Kasesela alitoa kauli hiyo wakati wa baraza la madiwani la halmashauri ya Wilaya ya Iringa vijijini lilipoketi mwishoni mwa wiki iliyopita katika ukumbi wa Siasa na Kilimo wakati akijibu swali la mmoja wa madiwani Philemon Temaigwe wa kata ya Ulanda aliyetaka kujua ni lini uvuvi haramu na uvuaji wasamaki wadogo utakomeshwa.
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa vijijini wakisali kabla ya kuanza kikao,
  “Hali hii ya kuvua samaki wadogo katika bwawa la Mtera inasababisha samaki washindwe kuzaliana kwa kuwa vizazi vya samaki vinauwawa, hivyo naagiza watendaji na afisa uvuvi kushughulikia hali hii kwa kuwakamata wavuvi wote na kuwanyang’anya samaki wadogo na kisha kuwapeleka katika vyombo vya sheria.” Alisema
 Kasesela alisema wapo baadhi ya wenyeviti wa vijiji wanaoshiriki biashara ya uvuvi haramu na kuwaagiza watendaji wa vijiji na vitongoji na wenyeviti wao kukomesha uvuvi haramu na kwamba yeyote atakayekamatwa akiwa na nyavu haramu au samaki, mtendaji wake hatakuwa na kazi kwa kuwa ameshindwa kusimamia sheria.
Aidha alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali katika kutoa taarifa za wavuvi ambao wanakiuka sheria za uvuvi kwa kutumia vyombo haramu hasa katika matumizi ya nyavu na kuomba wawataje wale wote wanaosuka nyavu hizo kwani ndio chanzo kikubwa cha uvuvi haramu.
Awali akichangia katika baraza hilo diwani wa kata ya Ulanda, Philemon Temaigwe alisema kuwa serikali inatakiwa kubaini nini chanzo cha nyavu za kuvulia samaki zinaendelea kuwepo wakati serikali ina mkono mkubwa wa kuweza kubaini wanaosuka nyavu hizo. Alisema endapo bwawa hilo litaendelea kuhujumiwa kwa kuendelea kufanya shughuli za uvuvi haramu itafikia mahali wananchi wenyewe watayakimbia maeneo yanayolizunguka bwawa hilo kwa kukosa shughuli za kufanya.  Alisema ifike wakati zana haramu ziteketezwe kwani zikiendelea kukaa muda mrefu katika vituo vya polisi au ofisi za watendaji ni chanzo cha kiashiria cha kupiga dili kwani wengi wa wavuvi wanaweza tumia kukaa kwa muda mrefu kwa nyavu hizo kuchukua kwa njia ya rushwa.


No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.