IFAHAMU IRINGA -1


Iringa ni mji ambao uko kama kilomita 500 kutoka jiji la Dar es Salaam. Mji wa iringa ulianza  kujengeneka mwaka 1889 wakati wa utawala wa Wajerumani. Jina la Iringa lililotakana na neno la kihehe Lilinga likiwa na maana Boma. Wahehe ndio kabila la awali lililoishi sehemu hii. Hakika kwa miaka mingi ya nyuma watu kutoka pembezoni mwa mji huu ambao walikuwa wakielekea sehemu ambapo ipo hospitali ya mkoa, mahakama na zamani ofisi za serikali walikuwa wakisema wanakwenda Bomani, jina hili liliendelea mpaka miaka ya 60. Iringa ndio makao makuu ya mkoa wa Iringa. Mitaa ya Iringa ni yenye utulivu na watu wake hupenda sana utani, japo hakika ukiwaudhi hawasiti kuonyesha kuudhika si watu wa kuficha hisia zao za furaja au za kuudhika. Mji wa Iringa uko mlimani ukiuangalia mto Ruaha ambao hujulikana rasmi kama Little Ruaha. Neno Ruaha pia linatokana na kukosewa kwa matamshi ya wenyeji ambao walikuwa wakiuita mto wao Luvaha, yaani wa siku nyingi au wa toka enzi, kwani kila aliyezaliwa alihadithiwa kuwa mto huo ulikuweko. Mtu mzee huitwa Mvaha.
Soko la Iringa ndilo jengo la zamani zaidi lililojengwa na Wajerumani, sifa ziwafikie wanaIringa kwa kutolivunja soko hilo bali kuliboresha ili liiendelee kutunza historia ya mji huu mkongwe.
Iringa imezungukwa na ardhi yenye rutuba na hali yake ya hewa ni nzuri sana yenye ubaridi kiasi hasa miezi ya Mei, Juni na Julai. Mitaa maarufu Iringa ni kama vile Kihesa, Mkwawa, Mwangata, Mtwivila, Ilala, Makorongoni, Mivinjeni, Kitanzini, Mshindo, Gangilonga, Kwakilosa, Ipogolo na Mlandege. Mjini kuna usafiri wa aina mbalimbali zikiwemo bodaboda, Bajaj, daladala na taxi kama ilivyo katika miji mingi ya Tanzania.
Mji wa Iringa ulianzishwa hasa na Wajerumani baada ya kupata upinzani mkali wa utawala wao kutoka kwa Wahehe, hivyo wakalazimika kujenga ngome eneo hili ili kuzuia uasi kutoka kwa kabila la Wahehe ambao walichukia sana kutawaliwa. Chini ya uongozi wa Mkwawa ambaye alijenga ngome yake Kalenga, kama kilomita 14 kutoka ulipo mji wa iringa sasa, Wahehe walitoa upinzani mkali sana kwa wakoloni wa Kijerumani, na hata kuwashinda vibaya katika moja ya mapambano yaliyofanyika eneo la Lugalo. Jengo ambalo lilikuwa mahakama zamani kwa sasa ni jumba la kumbukumbu yalikuwa kati ya majengo ya kwanza kujengwa baada ya soko, pia jengo la zamani la polisi ni kati majengo ya enzi ya utawala wa Ujerumani.

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.