WATU 44 WAUAWA KWA MILIPUKO KANISANI


RAIS  wa Misri  Abdul Fattah al-Sisi ametangaza miezi mitatu ya hali ya hatari nchini mwake baada ya makanisa mawili ya Kikopt kushambuliwa kwa mabomu na watu 44 kuuwawa. Kundi la wanaojiita Islamic State (IS) wametangaza kuwa wao ndio walioratibu mashambulio hayo katika miji ya Tanta na Alexandria siku ya Jumapili ya Matawi. Kundi hilo limeonya kuwa kutakuwa na mashambulio mengine. IS ilisema kuwa mashambulio yalifanywa na watu wawili waliojitoa muhanga, mmoja alienda katika kanisa la St George's Coptic kaskazini mwa jiji la Tanta, ambapo watu 27 waliuwawa . Saa chache baadae polisi walimzuia muuwaji mwingine kabla hajaingia kanisa la St Mark la Alexandria, huyu akajilipua nje ya kanisa na kusababisha vifo vya watu 17 wakiwemo askari polisi kadhaa. Milipuko hii imekuja wiki chache kabla ya ziara ya Pope Francis, ambaye amepanga kwenda Misri kuonyesha kuunga mkono wakristo wa nchi hiyo. Asilimia kumi ya wananchi wa Misri ni Wakristu.
Uamuzi wa Rais Sisi unategemewa kupata upinzani kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu, kwani kuna maelfu ya wananchi wamekwisha kamatwa bila ya kufuata taratibu katika amri kama hiyo na wengi walidaiwa kuteswa na hata kupotea bila ya  kujulikana wako hai au la.

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.