SHULE YA MSINGI KIGONZILE KUFANYIWA UKARABATI

Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati akikabidhiwa msaada wa mifuko ya saruji kwa ajili ya ukarabati wa shule ya msingi Kigonzile na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC)  Tanzania Samwel Kamanga, wakati wakiangaliwa na Mkuu wa Wilaya Richard Kasesela, mwenye sweta la rangi ya chungwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC)  Tanzania Samwel Kamanga akimkabidhi kiasi cha pesa mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Ritta Kabati zilizochangwa na baadhi ya wadau walijitokeza kwenye ukarabati wa shule ya msingi Kigonzile

Baada ya kufanikiwa kukarabati shule ya msingi Azimio iliyopo Kata ya Mshindo, Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ritta Kabati ameanza kukabati shule ya msingi Kigonzile iliyopo Kata ya Nduli kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwapo Shirika la Bima la Taifa (NIC) ambao walijitokeza kusaidia ukarabati wa shule hiyo ya Kigonzile.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa vitakavyo tumika katika kukarabati shule hiyo, Kabati alisema kuwa ameamua kufanya shughuli za kijamii ili kuifanya jamii ya watu wa Iringa kuwa na Elimu iliyobora na kuweza kuwa na kizazi ambacho kitakuwa cha kimaendeleo.

"Mimi sipendi kuona watoto wa Iringa wanakuwa wafanyakazi wa kazi za ndani kwa watu kwenye pesa au wafanyakazi wengi najiuliza tu kwanini Iringa ndio chimbuko la wafanyakazi wa kazi za ndani? Nitapambana kuhakikisha Iringa inakuwa na wasomi wengi ili kupunguza utegemezi" alisema kabati

Kabati alisema kuwa kuna shule nyingi zimeharibika katika Manispaa ya Iringa hivyo atakikisha anatafuta wafadhili mbalimbali kila kona hapa nchini na nje ya nchi ili kuhakikisha kukarabatiwa kwa  shule zote ambazo chakavu.

"Hii ni moja ya shule ambazo tayari nimeanza kuitafutia wafadhili hivyo hata shule nyingine nitahakikisha nafanya kazi na serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Rais wetu mpendwa Dr John Pombe Magufuli" alisema Kabati

Aidha Kabati aliomba wananchi kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi kuleta maendeleo kwa kuwa wakiitegemeea serikali tu hawawezi kupiga hatua ya kimaendeleo kutoka hapa walipo na kuweza kufikia malengo ya juu kimaisha.

Lakini Kabati aliwaomba viongozi na serikali kutafuta wahisani mbalimbali kila mahali ili kuweza kufanikisha kufikia malengo ya kimaendeleo na kuacha kuwa tegemezi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Samwel Kamanga, alisema kuwa ameguswa sana na uchakavu wa shule ya msingi Kigonzile kwa hali iliyonayo hivyo amechangia mifuko 160 ya saruji kwa ajili ya ukarabati.

"Mimi nimesoma kwenye shule kama hii na ndio sababu leo hii nipo hapa kama Mkurugenzi, nimeguswa sana kutokana na jinsi hii shule ilivyoharibika na inahitaji fedha nyingi, narudi makao makuu ya shirika letu nitatoa jibu kwa namna gani nitasaidia kuiboresha na kuwa kama shule nyingine za watu binafsi" alisema Kamanga

Aidha Kamanga aliwaomba wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya taifa ili kuepukana na kupunguza gharama wakati wa majanga kwa kuwa hujui lini utakumbana na matatizo ni vyema wananchi wakajua pia umuhimu wa bima ya afya.

Nae Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela alimshukuru mbunge wa viti maalum Ritta Kabati kwa jitihada zake za kuleta maendeleo katika Mkoa wa Iringa kwa kufanya kazi nyingi za kijamii tofauti na wanasiasa wengine.

"Tukiwa na wabunge kama hawa basi nchi itapiga hatua kubwa ya kimaendeleo kwa kuwa watakuwa wachapakazi na sio waroho wa madaraka wala sio wapenda pesa basi tutatoka hapa tulipo na kufika kule tunako staili" alisema Kasesela

Ila Kasesela aliwaomba viongozi wa serikali na wananchi kutumia Shirika la Bima la Taifa  NIC kwa kuwa limekuwa inafanya kazi zake vizuri kuliko bima nyingine hivyo ni lazima kuitambua bima hiyo kwa kuwa ni ya uhakika tofauti na bima nyingine zilizopo hapa nchini.

Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Nduli mtaa wa Kigonzile waliwashukuru viongozi wa serikali, Shirika la Bima la Taifa, diwani pamoja na Mbunge wa viti maalum Ritta Kabati kwa Juhudi kubwa za kukarabati shule hiyo ya Kigonzile kwa kuwa ilikuwa katika wakati mgumu sana.

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.