DC KILOLO AWAFUNDA VIJANADC  Kilolo  akizungumza na wananchi wa kijiji  cha Kiwalamo

Mkuu  wa wilaya  ya Kilolo Asia Abdalah akivuka daraja la  mto  Lukosi ambalo serikali  imetenga milioni 239 kwa ajili  ya ujenzi wa daraja  hilo
NA DENIS MLOWE, KILOLO
VIJANA wilayani Kilolo wametakiwa kuacha tabia ya kulalamika na badala yake wazitumie fursa za kiuchumi zilizopo katika maeneo yao kubuni miradi mbalimbali na kufanya kazi kwa bidii ili jamii iweze kuwaheshimu na kuthamini kazi zao.
 
Wito huo umetolewa na mkuu wa wilaya ya Kilolo, Asia Abdalah wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kiwalamo, kata ya Idete tarafa ya Kilolo mkoani Iringa, alipokwenda kukagua na kuwaeleza wananchi kuhusu ujenzi wa daraja linalounganisha mto Lukosi na vijiji vya jirani ambapo imetengwa jumla ya shilingi milioni 239 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.
 
Asiah alisema kuwa vijana waachane na tabia ya kulalamikia ajira wakati uwezo wa kujiajiri wanao na hasa katika sekta ya kilimo ambapo kwa wilaya ya Kilolo hususani katika kijiji cha Kiwalamo hali ya hewa anaruhusu mazao yote kulimwa.
 
Alisema kwa sasa mambo yamebadilika sana kwani vijana wengi wamekuwa wakishinda vijiweni huku wakilalamikia serikali kuwa hakuna ajira wakati uwezo wa kufanya kazi katika sekta ya kilimo wanaweza hivyo wajiwekee fikra za kujiajiri.
 
Alisema kuwa kwa sasa vijana wanayonafasi kubwa ya kujiunga na vikundi mbalimbali vya maendeleo na kubuni miradi mbalimbali ambayo kupitia Halmashauri serikali iliagiza kutolewa asilimia tano ya mapato ya Halmashauri kwa vijana, ambazo zitawasaidia kuendelea mbele kwa kuwapa mitaji ili wafanikishe kujikwamua katika soko la ajira.
 
“Vijana acheni kulalamikia ajira, wengi wenu mna nguvu za kufanya kazi za kilimo ambazo ni ajira tosha kwa sasa kwa vijana, lakini mmekaa mnalaumu serikali, naomba sana fanyeni kazi na kazi kwa kujishughulisha na kilimo na undeni vikundi kwani, hivyo nawaasa kujiwekea malengo ya kujiajiri wenyewe ili muingine katika soko la ushindani” alisema Asia Abdalah
 
Akizungumzia ujenzi wa daraja hilo, Mkuu wa wilaya alisema kuwa serikali imekwishatenga fedha  za ujenzi wa daraja hilo na hadi kufikia mwakani wananchi watakuwa wamekwisha anza kutumia daraja hilo.
 
Kwa upande wao wananchi wa kijiji  cha  Kilawamo wameipongeza serikali kwa  kutenga  kiasi cha  shilingi  milioni 239  kwa  ajili ya  kuwajengea daraja  la mto Lukosi ambalo  limekuwa  ni kero  kubwa  kwao  hasa wakati wa kuvusha  wagonjwa .
 
Wananchi walisema  kuwa  wamekuwa wakipata  shida  kubwa  sana  kuvusha  wagonjwa kwa machela katika daraja  hilo  ambalo ujenzi  wake  ulikwama kuendelea  kwa  zaidi ya  miaka saba sasa tangu lilipobomolewa na mvua.
 

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.