LEO NI MIAKA 100 TOKA WATOTO WA FATIMA, WAPATE MAONO YA MAMA MARIA


 
Jacinta, Francisco Marto, Lucia dos Santos
LEO inatimia miaka 100 toka watoto watatu huko Portugal walitoa taarifa kuwa wamemuona Bikira Maria, wakati wanachunga kondoo huko Fatima, kuanzia hapo watoto hao wamekuwa wakijulikana kama Watoto wa Fatima. Katika kuadhimisha hili kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki, siku ya Ijumaa Papa Francis alitua Lisbon na kisha kuanza kuzunguka mji huo kutumia gari lake linalojukana kama ‘Popemobile’ na kukutana na mamia ya waumini waliotoka sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya kuadhimisha miaka hiyo, inategemewa zaidi ya waumini milioni moja watashiriki. Kuna waumini wametoka nchi za mbali kama China, Venezuela na East Timor. Usiku katika kanisa ambalo limejengwa sehemu ambayo, Bikira Maria aliwatokea watoto hao wa Fatima, kulikuwa na mkesha uliotumia mwanga wa mishumaa tu, Papa aliongelea tatizo la vita zinazoichana dunia. Papa ataondoka Fatima baada ya misa leo Jumamosi na kumaliza ziara hiyo ya saa 24. Watoto wawili kati ya watatu waliotokewa na tukio hilo watatangazwa Watakatifu baada ya miujiza inayosemekana ilitokea kupitia wao. Moja ya sharti la kanisa Katoliki kutangaza mtu kuwa Mtakatifu lazima kutokee miujiza ambayo inasadikiwa imetokea kwa ajili ya mtu huyo. Hivyo Jacinta na Francisco Marto wataingia katika kundi la Watakatifu wa kanisa Katoliki. Hawa wote walifariki kwa ugonjwa wa Flu iliyoikumba Ulaya kati ya mwaka 1918-1919.
Kanisa Katoliki linathamini sana maono ya watoto hawa, kwani huaminika kuwa Bikira Maria alitoa maelekezo yaliyosaidia binadamu. Maono ya kwanza yalionekana tarehe 13 May mwaka 1917. Kulikuweko na kilichoitwa siri tatu za Fatima ambazo zilikuja kuandikwa na binamu yao

Lucia dos Santos, aliyefariki mwaka 2005 akiwa na umri wa miaka 97. Ambae nae taratibu za kuingia katika kundi la Watakatifu zilianza mwaka 2008. Siri hizo tatu ni zipi?

Hizi ni siri zilizoandikwa na Lucia miaka mingi baada ya maono aliyosema waliyaona. Lucia alijiunga na utawa katika konventi ya Coimbra. Siri mbili za kwanza za Lucia zilitolewa mwaka 1942,

·      siri ya kwanza ilikuwa ikielezea sura ya motoni ambako kuna bahari ya moto unaounguza roho za binadamu na mapepo

·      Siri ya pili ilikuwa ikielezea kuwa vita ya kwanza ya dunia itaisha lakini kungekuweko na vita ya pili ya dunia ambayo ingeanza wakati wa uongozi wa Papa Pius XI. (na ikatokea kama ilivyotabiriwa). Pia kulikuweko na ombi kuwa ni muhimu Urusi kuanza kuabudu Mungu au la nchi hiyo italeta maangamizi dunia nzima, na kuleta vita

·      Lucia alikabidhi bahasha ya siri ya tatu huko Vatican mwaka 1957. Mwaka 2000 barua hii ilisomwa kuwa ilieleza kuwa siri ya tatu ilielezea malaika akiomba wanadamu watubu dhambi zao, na kufanya malipizi, halafu ikaonyesha Papa na viongozi wengine wa dini wakipanda mlima, lakini wakiwa wanauwawa na askari waliokuwa wakitukia bunduki na mshale. Kanisa Katoliki limeelezea maono haya kuwa yanahamasisha watu kubadili mwenendo na kufuata njia zilizosahihi. Ikumbukwe pia kuwa Papa John Paul II alipigwa risasi tarehe 13 May 1981, waumini huamini kuwa Bikira Maria ndie aliyekwepesha kifo chake, na siri ya tatu ilikuwa inatabiri kupigwa kwake risasi. Papa John Paul alikabidhi risasi iliyotaka kumuuwa kwenye kanisa la Fatima.

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.