MHE. PHILLEMON NDESAMBURO AFARIKI DUNIA GHAFLA, RAIS ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI


Mbunge wa zamani wa Moshi mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Mheshimiwa Phillemon Kiwelu Ndesamburo, amefariki dunia ghafla leo 31 Mei, 2017 huko Moshi. Mtoto wa Ndesamburo amesema kuwa baba yake alidondoka ghafla ofisini kwake na kufariki papo hapo. Madaktari waasema alikuwa na tatizo kubwa la moyo. Mhe. Ndesamburo alizaliwa 19 Februari 1935, na alikuwa mbunge wa muda mrefu wa jimbo la Moshi Mjini, na pia alikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Kilimanjaro. Wakati huohuo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya MarehemuNdesamburo, viongozi na wanachama wa CHADEMA, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na kifo hicho. Mheshimiwa Rais katika salamu zake hizo alisema, “Kwa masikitiko nimepokea taarifa za kifo cha Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Moshi Mjini, Mzee wangu Philemon Ndesamburo kilichotokea leo tarehe 31 Mei, 2017 katika hospitali ya rufaa ya KCMC iliyopo Moshi Mkoani Kilimanjaro, namkumbuka Mzee Ndesamburo kwa hekima zake na uongozi wake uliozingatia siasa za kistaarabu”
Pia Mhe. Rais Magufuli amesema alifanya kazi na Marehemu Philemon Ndesamburo wakati wote wakiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wakati wote walishirikiana, kutaniana na anamkumbuka kwa namna ambavyo alitumia muda wake bungeni kupigania mambo yenye maslahi kwa wananchi wa jimbo lake la Moshi Mjini.
Mhe. Dkt. Magufuli ameitaka familia ya Marehemu Philemon Ndesamburo na wote waliguswa na msiba huu kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu na amemuombea Marehemu apumzishwe mahali pema peponi, Amina.

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.