TIMU 43 KUSHIRIKI KOMBE LA MBUNGE RITA KABATI


Mdhamini Rita Kabati, akikabidhi vifaa vya soka
MASHINDANO ya kugombea kombe la mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Rita Kabati (CCM), yatakayoshirikisha timu 43 yamepangwa kuanza kutimua vumbi katika  viwanja vinne tofauti Mei 28 mwaka huu.
 
Mmoja wa waratibu wa mashindano hayo, Fred Mgunda’ Mkurugenzi’ alisema mashindano hayo yamepangwa kwa kufunguliwa rasmi Mei 28 katika uwanja wa Ipogoro  na yatajulikana kwa jina la Rita Kabati Challenge Cup na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Michezo au Naibu wake na kuhudhuriwa na wachezaji Zaidi ya 1000 watakaoshiriki mashindano hayo.
 
Mgunda alisema kuwa lengo ya mashindano hayo ambayo yamedhaminiwa na Mbunge Kabati, ni kuibua vipaji na kukuza vipaji vya vijana kuweza kuwapata wachezaji ambao watakuwa wawakilishi wazuri katika timu zinazoshiriki ligi nchini endapo wataamua kufatilia vipaji mikoani.
 
Alisema mashindano hayo kwa mara ya kwanza katika historia ya mkoa wa Iringa yatashirikisha timu nyingi zaidi na yatakuwa katika mtindo wa mtoano katika hatua za awali na zikibaki timu nane kutakuwa na makundi mawili yenye timu nne ambapo washindi wawili katika makundi wataingia hatua ya nusu fainali.
 
Alisema kuwa viwanja vitakavyotumika katika mashindano hayo ni viwanja vya Mlandege, Ipogolo uwanja wa Kleruu kwa upande wa Iringa mjini na uwanja wa Wambi wa mjini Mafinga utatumika kwa timu za wilaya ya Mufindi na uwanja wa Ismani kwa timu za wilaya Iringa vijijini.
 
Aliongeza kuwa katika mashindano hayo kila timu watapatiwa jezi za mashindano kutoka kwa mdhamini wa mashindano hayo Rita Kabati na zawadi za washindi wa kwanza hadi wa tatu, mchezaji bora wa mashindano, mfungaji bora na kikundi bora cha ushangiliaji kwa timu zinashiriki watapatiwa zawadi.
 
“Mashindano haya kila mwaka yatakuwa na motisha mpya kwa wachezaji na timu husika kwani ndio kwanza yameanza kwa mujibu wa mdhamini yanatarajia kuwa ya kila mwaka na yatafata kanuni zote zinazo ongoza mpira wa miguu duniani hivyo kanuni na sheria lazima zifatwe na timu husika” alisema
 
Mgunda alizitaja zawadi ambazo zitatolewa kwa mshindi wa kwanza kuwa ni pikipiki yenye thamani zaidi ya shilingi milioni 2, kikombe, mpira na medali, mshindi wa pili ataondoka na kikombe na shilingi 500,000 na mshindi wa tatu ataondoka na shilingi 200,000, Kikundi bora 100,000.

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.