TUCHEKE KIDOGO-LAZIMA NIMSHTAKI MTU


Mimi sielewi kabisa kosa langu na jambo hili lazima nilifikishe kwenye vyombo vya dola. Nchi hii ni nchi yenye amani ambayo mtu unaruhusiwa kwenda popote mradi huvunji sheria, na unaruhusiwa kufanya chochote mradi huvunji sheria, na mimi sijavunja sheria yoyote lakini kundi la wapiga debe wa pale Ubungo wamejichukulia sheria mkononi na hapa nilipo shati limechanika, kila nilichokuwa nacho mfukoni kimechukuliwa, mpaka ufunguo wa geto langu, uso umevimba na nina wasi wasi kuna meno yameng’oka maana nasikia maumivu makali sana mdomoni. Jamani kwanini mateso haya wakati sina kosa lolote? Mkasa mzima ulikuwa hivi. Baada ya kumaliza shughuli zangu pale Manzese nikaona nielekee nyumbani kwangu Ubungo. Kwa vile hali ilikuwa ngumu kidogo, hivyo basi sikupanda daladala wala mwendokasi nikaanza kutwanga mguu polepole. Hakuna aliyanisalimu wala kunisumbua, si unajua Bongo ilivyo kila mtu na shughuli zake. Nilipofika karibu na kituo cha mabasi ya kwenda mikoani, mambo yakabadilika, nikajikuta nasalimiwa na watu wengi tu, kila mmoja akiwa ananikaribisha nisafiri nae ‘Mbeya Kyela saa kumi na mbili twende’, mwingine akanishika mkono, ‘Twende Tabora mzee basi safi lakshari’ mwingine kaniomba twende Moshi Arusha, mwingine Njombe, basi shida tupu, nikimkatalia huyu kuwa sisafiri  anakuja mwingine.  Mwishoni akaja dada mmoja mrembo akanisalimia, ‘Kaka hujambo?’ Nikaona hili ni zali, nikajibu kwa tabasamu la kuonyesha nimempenda ‘Sijambo mrembo’. Akanambia ‘Njoo ofisini kwetu’, nikaona nafasi kama hizi hutokea mara chache sana, si rahisi msichana mrembo kukusimamisha barabarani na kukukaribisha kwake mji huu. Kimoyo moyo nikajisema Mungu hamtupi kiumbe chake. Haraka nikaanza kumfwata. Wapiga debe wakaendelea kunibembeleza nisafiri nikawa naendelea kuwakatalia huku ninamfwata huyu mrembo aliyeonekana kunipenda mwenyewe. Wahenga walisema fwata nyuki ule asali. Tukaingia ndani ya ofisi moja ya kukatia tiketi, binti akachukua kitabu cha tiketi na kwa sauti tamu ileile akaniuliza ninakwenda wapi. Nami kwa sauti ya mapenzi nikamjibu, ‘Naelekea Ubungo mpenzi’. Ghafla ilikuwa kama kimya fulani kimeingia kwenye ofisi ile, ‘Yule binti akaniuliza kwa sauti ya mshangao,  ‘Umesemaje?’ Nikarudia kuwa naelekea kwangu Ubungo, likaanza zogo, nikaanza kuulizwa nani kanambia pale zinapatikana tiketi za Ubungo? Wengine wakiuliza kwanini natania kazi zao, yule dada aliye nileta pale ndio alikuwa mkali zaidi akidai nimempotezea muda wake, nikajitetea kuwa nilidhani kanipenda ananiita ofisini tuongee ndipo hapo walipoanza kunishushia kipondo……

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.