VIJANA WA IRINGA HUENDA WAPI KUPUMZISHA AKILI BAADA YA SAA ZA KAZI?

Iringa ni mji mkubwa ambao kwa sasa una watu zaidi ya laki mbili, wengi wao wakiwa vijana, lakini kama ilivyo katika miji karibu yote kuna tatizo kubwa la kukosekana kwa eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya shughuli za sanaa na burudani zitokanazo na sanaa. Kwa ujumla si utamaduni wa viongozi wa Tanzania kuhamasisha kutengwa maeneo maalumu ya sanaa, japo ni jambo la kawaida kabisa viongozi haohao kusikika wakihamasisha kutengwa maeneo ya michezo. 
Ni jambo la ajabu lakini ni kweli kuwa pamoja na wakoloni kulaaniwa kuwa walikuwa ni chanzo cha kuuwa utamaduni, ukweli ulio wazi kuwa wakoloni walifanya mambo mengi tu yaliyosaidia kulinda na kuendeleza  utamaduni wa Iringa. Na bila shaka baada ya Uhuru, uongozi unaotokana na sisi wenyewe, ndio ambao umekuwa mstari wa mbele kudharau na hivyo kupoteza utamaduni wetu. 
CHIEF ADAM SAPI MARA BAADA YA KUPOKEA FUVU LA MKWAWA 1954
Ngoja nianze na mifano midogo, ni jambo lililo katika historia kuwa ni wakati wa ukoloni ambapo juhudi za kurudisha fuvu la Mkwawa lilipofanyika, na hata kujengwa kwa eneo la kutunzia fuvu hilo kulifanyika wakati huo. Fuvu lilirudishwa mwaka 1954, Je, ni kwa kiasi gani eneo lile ambapo fuvu la mtu huyu mwenye historia kubwa katika kabila la Wahehe limeboreshwa kuanzia mwaka 1954? Je ni jitihada gani zinafanywa ili vizazi vya sasa vielewe umuhimu wa mtu huyu katika historia ya Iringa na ya Tanzania? Minara ya kumbukumbu kama ule wa kaburi la Von Zelewisky pale Lugalo inaongezewa thamani kiasi gani kuhakikisha historia haipotei? 
Wakati wa mkoloni ndipo kulijengwa sehemu maalumu za burudani, zikiwemo ukumbi ulioitwa Welfare Center au Community Center, hapa ndipo yalipopigwa madansi, wanafunzi na vikundi mbalimbali vya sana vilionyesha michezo ya kuigiza, nje ya ukumbi huu kulikuwa na uwanja mkubwa ambapo pia ziliwekwa bembea na michezo mingine ya watoto, uwanja huu ulitumika usiku kwa maonyesho ya sinema za bure. Swali, Je, ukumbi huu uliojengwa wakati wa ukoloni kwa shughuli za sanaa, burudani, elimu kwa jamii, umefanyiwa maboresho gani toka ukoloni? Leo ni miaka 56 toka tumepata Uhuru. Ukumbi wa Welfare Center ulijengwa wakati mji wa Iringa una watu kiasi cha 10,000, leo Iringa ina zaidi ya watu laki mbili, Nini kimefanyika kukahakikisha watu hawa wanasehemu ambayo ni ya burudani lakini si lazima iambatane na ulevi? Sehemu gani ambayo watu hawa  wanaenda kupumzisha akili zao bila kukutana na ulevi? Je hawa vijana wa Iringa baada ya kufanya kazi mchana kutwa au kusoma mchana kutwa, huwa wanaenda wapi kuburudisha akili zao? Mara nyingine uongozi huanza vita za kukabiliana na ulevi na mambo mengine mabaya lakini bila kujiuliza maswali haya ya msingi. Hawa vijana wanapewa fursa gani za kufurahia ujana wao baada ya saa za kazi zaidi ya kuishia kwenye ulevi au guest house? Sehemu za ulevi ziko nyingi sana tena zimetengewa maeneo makubwa, wapi sehemu ambazo mtu anaweza kwenda kucheza bao karata, kusikiliza muziki, kuangalia sinema au michezo ya kuigiza bila kulazimika kuingizwa kwenye vishwawishi vingine?
Katika mipango ya mji wa kisasa ni uhimu kupanga maeneo ya kupata nafasi kupumzisha akili, swala la kuona watu wote wanapenda michezo au wanashiriki michezo tu, ni kujitoa ufahamu kwani si kila mtu anapenda kucheza au kuangalia mpira, hakika hata sensa ya waangaliaji wa mpira ingefanywa ingeonyesha asilimia ndogo sana ya watu huenda mpirani. Miji yote ya maan duniani huwa na Town Hall, ukumbi wa serikali ya mji ambao unaweza kutumika mwa mambo mbalimbali.
Kwa neng'ino sinzile kulonga

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.