HISTORIA YA JOHN KITIME -1

NIMO katika hatua za mwisho za kukamilisha kitabu cha maisha yangu, nia ya kuandika maisha yangu hasa inahusu kuelezea Iringa ilivyokuwa wakati nakua, wana Iringa waweze kupata japo vionjo vya mji ulivyokuwa miaka kati ya 1961 na 1999. Hapa nitaleta mkhtasari wa yale yaliyomo katika kitabu;

Nimezaliwa Iringa, wazazi wangu wote walikuwa waalimu. Baba alikuwa Headmaster (mwalimu mkuu) wa Iringa Middle School, (iliyoitwa baadae Mshindo Primary School), shule ambayo wenye akili fulani katika miaka ya sabini, waliamua ivunjwe ili ujengwe uwanja wa michezo, na ndipo ukapatikana uwanja wa Samora. Middle School ilikuwa ndio shule inayofuata baada ya mwanafunzi kumaliza Government Primary School, shule ambayo sasa inaitwa Mlandege Primary School. Hizi zilikuwa shule za serikali,  Government Primary School ilianza darasa la kwanza hadi darasa la nne, na Middle School ilianzia darasa la tano hadi darasa la nane.
Government Primary School, madirisha matatu kushoto darasa 1a, na 1b
Mama alikuwa anafanya kazi iliyoitwa Mama maendeleo, ofisi yake ilikuwa katika jengo la Welfare Center Kitanzini, jengo ambalo wenyeji waliliita Olofea senda, jengo hili ambalo pia liliitwa Community Center au Jumba la Maendeleo, lilikuwa mahala walipokusanyika watu mbalimbali , vikundi vya akina mama vilikuwa vikifundishwa na mambo mbalimbali ikiwemo upishi, ususi, ushonaji, ufinyanzi na kuweza kujipatia fedha kwa shughuli hizi. Kwa siku hizi wangeitwa wajasilia mali. Pia katika jengo hili lilitumika kama kituo cha bure cha watoto wadogo. Watoto wa akina mama waliokuwa wanakuja kufanya ujasilia mali na watoto wa jirani na jengo hili walikusanywa hapa na kufundishwa kuimba, na hâta kusoma na kuandika, ilikuwa ni aina ya nursery school mwalimu wao alikuwa Mzee Mwambola. Wasanii mbalimbali walikusanyika hapa mchana kufanya mazoezi ya kwaya, bendi, michezo ya kuigiza na kadhalika, na pia palikuwa na michezo kama bao na boxing. Palikuwa ni mahala palipochangamka mchana na usiku, kulikuwa na maonyesho ya michezo ya kuigiza iliyofanywa hapa na madansi yalipigwa hapa nyakati za usiku. Nje ya ukumbi kulikuwa na uwanja ambao mchana ulikuwa ni sehemu ya kucheza watoto, ilikuwa pia na mabembea na ya chuma, bahati mbaya uwanja huo sasa umekuwa gulio la kuuzia mitumba, sijui watoto wamepewa uwanja gani mbadala. Mara  moja kwa mwezi kulionyeshwa sinema ya bure katika uwanja huu.
Kwa kuwa baba alikuwa mwalimu mkuu wa Middle School, alikuwa na nyumba palepale jirani na shule, hivyo basi shule iliyokuwa karibu kwa ajili yangu ilikuwa ni Government Primary school, maarufu kwa jina la Gavamendi. Nilianza darasa la kwanza 1961 Government Primary School, darasa la kwanza lilikuwa na  makundi mawili 1A, na 1B. Mimi nilikuwa 1B, mwalimu wetu wa darasa alikuwa Mwalimu Chitigo, mwalimu wa darasa la 1A alikuwa Mwalimu Mary. Ratiba za darasa la kwanza zilikuwa tofauti na zile za madarasa mengine, darasa la kwanza lilianza vipindi saa nne, ili kuwa na ishara tofauti, madarasa ya juu yalibadilisha vipindi kwa ishara ya kengele, darasa la kwanza walibadilisha vipindi kwa kupigiwa pipa. Mwalimu Mkuu wakati huo alikuwa mwalimu George Nyakunga. Namkumbuka Mwalimu George akituita na kutugawia uniform zetu ambazo siku hizo zilikuwa zinashonwa na fundi maalumu wa shule. Kaptura ya kitambaa cha Kaki, na shati ambalo lilikuwa na shingo ya mviringo bila kola, wala vifungo, likifanana sana na Tshirt za siku hizi. Kumbukumb za darasa la kwanza nilizonazo ni kujifunza kuandika na hesabu, na pia hadithi nyingi na nyimbo za mwalimu Chitigo, wakati huo tukihadithiwa hadithi za mazimwi tuliamini kabisa kuwa duniani kuna mazimwi. Kati ya mambo ambayo yalitutisha sana kipindi hicho ni pale ulipozuka uvumi kuwa choo kimoja cha wasichana kina jini. Hii ilitusumbua sana wavulana kwani ili kufika choo cha wavulana ilikuwa lazima upite choo cha wasichana, woga huu ulikuja kupungua siku mwalimu mkuu alipotuambia kuwa kuna mbuzi katolewa sadaka hivyo jini kaondoka, nadhani ilikuwa ni hadithi tu ya kutuweka sawa. 
Choo chenye milango ya bluu cha wasichana, nyuma yake choo cha wavulana
Nilisoma shule hiyo kwa miaka miwili kisha nikahamia Consolata Primary School, shule ambayo sasa leo inaitwa Shule ya Msingi Chemchem. Shule hii ilikuwa ikimilikiwa na kanisa Katoliki. Sababu za kuhama ni kuwa nilianza kuishi na babu yangu aliyekuwa akiishi Makorongoni, mtaa wa Barabara mbili. Nyumba ya Kilabu maarufu cha Barabara mbili ndiyo ilikuwa nyumba ya bau yangu Mwalimu Raphael Kitime.
Mtaa wa barabara Mbili
Kwa siku hizi nyuma tu ya barabara mbili ndipo ilipo stendi kuu ya mabasi Iringa, wakati huo hapo palikuwa na makaburi, ambayo yalipakana na makaburi ya wahindi, walipokuwa wakichoma maiti zao. Utotoni hatukujali kuwa palikuwa makaburi muda mwingi tulikuwa tukicheza humo.
 
Wakati huo shule ya Consolata ilikuwa na walimu wengi wakiwemo mwalimu Daudi Luhanga, Mwalimu Kalinga, Mwalimu Filangali, Mwalimu Mkuu akiwa Mwalimu Mwinuka, na ni katika wakati huu ndipo naweza kusema dhahiri kuwa hamu ya muziki ilijijenga moyoni mwangu.…itaendelea

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.