IS WAFANYA SHAMBULIO LA KWANZA IRAN


Mashambulio mawili ya kigaidi kwenye jengo la Bunge la Iran, na kwenye kaburi la Ayatollah Khomeini katika mji mkuu wa Iran, Tehran, yamesababisha vifo vya watu 12. Kadri ya maelezo ya vyombo vya usalama vya Iran, magaidi wote wameuwawa.  Kundi la IS limesema linahusika na mashambulio hayo. kama ni kweli hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa kundi la IS kufanya shambulio la aina yoyote ndani ya Iran.  Wakati huohuo Revolutionary Guards wa Iran wametoa taarifa wakizituhumu Saudi Arabia na Marekani kwa kuhusika na shambulio hilo.
"Kitendo cha shambulio kufanyika wiki moja baada ya mikutano kati ya Rais wa Marekani na viongozi wa serikali ya Saudi Arabia, inaonyesha kuwa wao wanahusika ," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa upande wake Marekani imelaani shambulio hilo ikisema ugaidi hauna nafasi katika dunia yenye amani na ustaarabu.
Rais Hassan Rouhani wa Iran alitoa ujumbe na kusema , ugaidi ni tatizo la dunia nzima, na akasema kunahitajika ushirikiano na umoja wa kimataifa.  Wakati huohuo Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema mashambulio hayo hayata badilisha chochote Iran. IS wametoa taarifa kuwa watafanya tena mashambulio dhidi wa Shia walio wengi katika nchi ya Iran.  Kwa maelezo ya walioshuhudia, magaidi hao waliingia kwenye jengo la Bunge kupitia mlango mkuu wakiwa wamevaa kama wanawake. Walipoingia walitoa bunduki aina ya Kalashnikov, na ndizo walizotumia, lakini majeshi ya usalama yakazingira jengo hilo, na magaidi wanne waliokuwa katika jengo hilo hatimae wakauwawa.  Wakati huohuo pia lilifanyika shambulio la kwenye kaburi la muanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ayatollah Khomeini, magaidi walianzisha mashambulio kwa kuanza kufyatua risasi hovyo, mmoja wa washambuliaji akajilipua na mwingine akauwawa na askari wa usalama. Inasemekana aliyejilipua alikuwa mwanamke.

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.