TAMKO LA RAIS KUHUSU WANAFUNZI WALIOPATA MIMBA LALETA MJADALA

Tamko la Rais John Pombe Magufuli wiki hii kuwa wasichana ambao watapata mimba wakiwa shuleni hawataruhusiwa kuendelea na shule kwenye shule za serikali limeanzisha mjadala mkali, nchini na nje ya nchi kukiwemo na makundi ya pande mbili, wanaomuunga mkono na wale wanaopinga, kauli hiyo. Kwa utafiti wa Human Rights Watch Report , wastani wa wasichana  8,000 huacha shule kila mwaka kutokana na kupata mimba.
 Kundi la wanaopinga kauli ya Rais wanasema kuwa, kwanza ni haki ya kila mtu kupata elimu,  hivyo kumnyima elimu mtu kwa sababu yoyote ni kukiuka katiba. Wengine wakidai kuwa vita ya kumkomboa msichana wa Kiafrika ilikuwa inaendelea vizuri, wanaona Rais amegeuka na kuwasaliti. Pia wanakumbusha kuwa si mara moja ambapo viongozi wengine wa serikali ya Magufuli  wametamka kutetea haki ya kuendelea na masomo wasichana ambao wamejikuta wamepata mimba.
Kwa upande wa pili wako wale wanaotetea kwa nguvu kauli ya Rauis wanaosema watoto wa shule hawatakiwi kujihusisha na mambo ambayo yanasababisha wapate mimba. Wako wanaoangalia upande wa imani ya dini unaokataza kabisa kujihusisha na mapenzi kwa watu walio nje ya ndoa. Mwalimu mmoja alisema wasichana wakishazaa ni vigumu kuheshimu sheria za shule kwani wanajiona wamekwisha kuwa watu wazima. Na wengine wakitetea mila na desturi za asili ambazo hazikubaliana na binti kupata mimba nje ya ndoa.

Mjadala huu hakika hautakuwa mfupi, kwani kwa wengine pia unaonekana ni taratibu zinazolamishwa kuingizwa katika jamii yetu kutokana na ushawishi wa nchi za magharibi, zikilinganishwa na  kampeni za kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja. Kumekuweko na mawazo kuwa taasisi ambazo zinatetea mabinti waliozaa kuendelea na elimu,  watafute misaada ya kufungua shule zitakazoshughulika na wanafunzi waliozaa, kwani inaonekana watetezi wa wasichana katika kundi hili hawaangalii athali zitakazowapata wanafunzi ambao hawajazaa.

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.