WANACHUO WAWASAIDIA KITUO CHA WATOTO YATIMA SABASABA

NA DENIS MLOWE, IRINGA
 
WANACHUO wa Kitivo cha Biashara na Uchumi wa chuo Kikuu cha Iringa wametoa msaada kwa watoto yatima katika kituo cha Upendo Center kilichopo Sabasaba, manispaa ya Iringa ambacho kimejitolea kulea watoto yatima na watu wasiojiweza tangu mwaka 1994.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa kamati ya Uratibu wa Msaada huo mwanachuo kutoka kitivo cha Biashara na Uchumi mwaka wa pili, Holo Simba alisema kuwa lengo la msaada huo ni kuungana na watoto katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani na kujumuika pamoja na kuwapatia faraja ambayo itawafanya waone jamii bado iko nao sambamba. Alisema kuwa baada ya kukaa kikao waliamua kwa pamoja kujitolea vitu mbalimbali kuliko kuendelea kutumia vitu hivyo kwa anasa ni bora wajichangishe kuweza kuwapatia mahitaji watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
Holo aliongeza  kuwa kwa kupitia utaratibu waliojiwekea kila mwaka kutoa misaada kwa watoto yatima mwaka huu wameguswa kuwasaidia vitu mbalimbali watoto wanaishi katika kituo cha Upendo Center ni kutokana na mahitaji ambayo wameona bora watoe kwa kituo hicho kwa kuwa kuna vituo vingi mkoani hapa lakini kituo cha Sabasaba kinasaulika na watu wengi licha ya kuwa moja ya vituo vikongwe mkoani hapa. Simba alisema kuwa jamii inapaswa kutambua na kujitoa katika kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kuwajali kwa kila namna ili waweze kuishi kwa upendo kama ambapo wangekuwa katika familia zao.
Alisema kuwa wamefanikiwa kuwapatia msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo nguo, mafuta sabuni, vyakula, peni kalamu na madaftari vyote na pia kula pamoja chakula ambacho kilipikwa na wanafunzi wa kitivo cha biashara na uchumi ambapo vyote vikiwa na zaidi ya thamani ya shilingi 600,000
“Japo msaada sio mkubwa sana kukidhi mahitaji ya watoto yatima,bali itasaidia kidogo kufanya watoto wajisike wapo kama watoto wengine wenye wazazi kwani kutoa ni moyo hivyo ni wakati huu wa Ramadhani kuna umuhimu mkubwa sana kwa watu kujitolea vitu mbalimbali kwa watoto hawa” alisema. Naye mkuu wa Idara wa Kitivo cha Biashara na Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Iringa, Mwalimu Mlasu Serijo alisema kuwa msaada huo umekuja kutokana na changamoto nyingi ambazo wanakabiliana watoto wanaishi katika kituo cha Upendo Center. Alisema kuwa watoto yatima ni wahanga wa matatizo yetu  katika jamii ndio maana wapo hivyo sio jukumu la serikali pekee kuwahudumia watoto hawa kutokana na umuhimu wao katika jamii kwani ndani yao kuna watoto
watakaokuja kuwa kuwa maProfesa, madaktari bingwa na wanasheria hivyo kuwatembelea ni njia mojawapo ya kuwafanya wapate moyo wa kusoma zaidi na kujitoa. Alisema kuwa watoto hawa wengi wao ni watakuwa moja ya nguzo za taifa hapo mbeleni hivyo upendo juu yao ni muhimu sana kwa jamii yote kwani ni kitendo cha MUNGU kuweza kuwatembelea hawa watoto na kuweza kutenga sehemu kidogo alichonacho kutoa kwa watoto.
Kwa upande wake Mlezi wa kituo hicho Hilary Konyaki aliwashukuru wanachuo hao chuo kikuu cha Iringa kwa msaada huo ambao umekuja kwa wakati mwafaka na kuwataka wadau wengi zaidi wajitokeze kukisaidia kituo hicho kwa kuwa hakina wafadhili zaidi ya michango mbalimbali kutoka kwa jamii na majirani.
Alisema kuwa kituo hicho kimefanikiwa kuwatoa watoto wengi zaidi ya 1000 tangu kuanzishwa kwake ambao wengine wamekuwa wasomi wakubwa nchini na kwa sasa kina watoto 32 ambapo wa kike ni 12 na wakiume 20 ambao wanapata huduma mbalimbali kituoni hapo.

 

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.