WATU 6 WAUWAWA KATIKA SHAMBULIO LA KIGAIDI LONDONWATU 6 wameuwawa katika  shambulio jingine la kigaidi katikati ya jiji la London, watu 50 wanasemekana wamejeruhiwa. Watu watatu kati wanaodhaniwa ni magaidi walipigwa risasi na polisi na kuuwawa hapohapo.  Gari aina ya minibus jeupe liliacha barabara na kuanza kuwagonga watu waliokuwa wakitembea pembeni mwa barabara, juu ya daraja maarufu la London Bridge kiasi cha saa nne usiku kwa saa za Uingereza. Baada ya kuwagonga watu kadhaa watu watatu walishuka kutoka kwenye hilo gari na kuanza kuchoma visu mtu yoyote waliyemkuta mbele yao. Ilichukua dakika nane tu kabla ya watu hao hawajapigwa risasi na kuuwawa na polisi. Taasisi ya London Ambulance Service imesema watu 48 walijeruhiwa na kupelekwa katika hospitali mbalimbali za jiji hilo. Madaktari zaidi ya 80 walipelekwa eneo la tukio kutoa huduma za matibabu kwa majeruhi. Mmoja wa majeruhi ni afisa wa British Transport Police, aliyechomwa kisu, amejeruhiwa vibaya lakini madaktari wanasema atapona. Kamishan Msaidizi wa Metropolitan Police  Mark Rowley alisema: "Magaidi walikuwa wamevaa majaketi yaliyokuwa yakionekana kama ni mabomu ya kujitoa mhanga, lakini ilikuja kugundulika kuwa yalikuwa mabomu feki." Hili ni tukio la 3 la ugaidi nchini Uingereza katika miezi mitatu iliyopita. Wiki mbili zilizopita watu 22 waliuwawa na kijana aliyejilipua nje ya ukumbi wa muziki huko Manchester. Waziri Mkuu wa Uingereza Bi Theresa May amesema ameitisha kikao cha dharura cha kamati ya usalama. Wakati huohuo Meya wa jiji la London Sadiq Khan amekiita kitendo hicho kuwa ni cha uwoga na cha kuwaonea wakazi wa London wasio na hatia. Mmoja ya watu walioona tukio wanasema minibus hiyo ilikuwa inakwenda kwa spidi ya kiasi cha kilomita 80 kwa saa, ikaacha barabara ghafla na kuanza kugonga hovyo watu waliokuwa pembeni ya barabara.

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.