BURUDIKA NA HISTORIA UA UHEHENI

Mkwawa alizaliwa mwaka 1855, katika utoto wake Mkwawa alianza kujifunza mambo ya kivita kutoka kwa baba yake Munyigumba, ambaye alikuwa mpiganaji hodari aliyeweza kuteka sehemu kubwa ya nchi, pia Mkwawa akapata elimu ya vita kutoka kwa majemadari hodari wa jeshi la baba yake kama vile  Mutanilamadunda na Muvilimasasi na majemadari wengine. Mkwawa hatimae ndie aliyekuja kujulikana sana kwa kuwa ndie aliyekuwa Sultani wa mwisho wa aina yake Uheheni, kabla ya kuingia Wakoloni. Lakini kuna masultani wengi wa Wahehe waliomtangulia ambao nao walifanya makubwa sana na walikuwa wakiogopwa na majirani wao. Kwa mfano baba yake Mkwawa, Sultan Muyugumba ndie aliyeanza kuunganisha koo mbalimbali za Kihehe kuwa kitu kimoja.  Vilevile Mihwela wa Udongwe, mjomba wake Munyigumba alikuwa shujaa mkubwa sana kwani ndie haswa alieanza kujenga Uhehe moja.  Uhehe ilikuwa na watawala mbalimbali kila moja akijitegemea, kulikuwa na Udongwe, Luhota, Lungemba, Ng'uluhe, Malangali, Wota, Ndevela, Usagala, Uhafiwa na nyinginezo, Miwhela ndie aliyeweza kuziunganisha.
Licha ya kuwa Mkwawa alishakuwa askari mpiganaji hodari, baba yake alipofariki aliyetawazwa kwanza alikuwa Mwalevike, huyu hakuishi muda mrefu kwani aliuwawa na Mwamubambe Mwanakimamule Mwalunyungu, na baada ya hapo akatawazwa Muhenga, huyu alikuwa kibaraka tu wa Mwamubambe, Mkwawa alitimuliwa na akakimbilia  kwa nduguze Wota kama nilivyosimulia huko nyuma, baadae alirudi na kufanikiwa kumuua Mwamubambe ambaye historia inaonyesha alikuwa ni mateka kutoka jeshi la Wasangu ambae alipendelewa tu na Munyigumba kutokana na ubora wa umbo lake, hakustahili kutawala Uhehe.

Kati ya vita ambazo Mkwawa alishiriki;

  1. Vita na Wangoni: Mkwawa alikusanya jeshi na kwenda kuwapiga Wangoni waliokuwa wamemzingira baba yake katika mapango, alimuokoa baba yake na kisha kuwafukuza Wangoni mpaka Ubena.
  2. Vita na Wasangu: Akiwa na umri wa miaka 24 Mkwawa alitumwa na baba yake kuwapiga Wasangu. Mkwawa alikwenda vitani na majemadari maarufu Muvilimasasi, na Mutanilamadunda na kushinda vita ile.
  3. Vita kali ya Lundamatwe: alipopigana na Mwanakimamule Mwamubambe na kumuua na kurudisha utawala wake Uheheni
  4. Vita ya pili na Wangoni: Baada ya mapigano makali yaliyoendelea mpaka kingo za mtu wa Ruhuhu ikakubalika hakuna mshindi, makabila haya yakakubaliana amani wakiwa kule Ubena kando ya Bwawa la Itombololo karibu na Mdandu. Kwa vile walipigania katika ardhi ya Ubena wakakubaliana kugawana nchi hiyo, nusu kwa nusu Chaburuma wa Wangoni nusu na Mkwawa nusu. Ndio chanzo cha utani wa Wahehe na Wangoni.
  5. Mkwawa aliendelea kupigana na kuwateka Wambunga na Wadamba na akatwaa Bonde la Kilombelo kwa kumtumia jemadari wake Mutanilamadunda.
  6. Ugogo na Usagala zilijisalimisha chini ya Mkwawa  akiwa na jemadari wake Musangila Mwamufilinge
  7. Wahehe na Wahuma ( Vahumba/Wamasai) walipigana mara kwa mara, hasa kutokana na maadui hao kuwa na tabia ya kuiba mifugo, mara zote Wahehe walishinda vita hizo.  Kwa mfano Mihwela aliwahi kuwapiga Wahumba huko Lyambangali. Lakini kuliwahi kuwa na pambano kali sana la makabila haya kule Image kiasi cha kwamba hakubaki mwanaume hata mmoja. Vita ya mwisho ya Wahehe na Wamasai ilitokea Guluwe Mpwapwa, Wahehe wakiongozwa na Msambapakafu, Wamasai walishindwa vibaya hawakurudia tena kuchokoza Wahehe. Katika vita ya na Wakimbu na Wanyamwezi chini ya Kiyungi, washindi walikuwa Wahehe, Ukimbu na Unyamwezi zikawa chini ya himaya ya Uhehe. Mkwawa alimuweka Mgonapakilo Mwakalolo kuwa Mnzagila wa Wakimbu....itaendelea


No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.