HISTORIA YA JOHN kITIME II

NIMO katika hatua za mwisho za kukamilisha kitabu cha maisha yangu, nia ya kuandika maisha yangu hasa inahusu kuelezea Iringa ilivyokuwa wakati nakua, wana Iringa waweze kupata japo vionjo vya mji ulivyokuwa miaka kati ya 1961 na 1999. Hapa nitaleta mkhtasari wa yale yaliyomo katika kitabu;
Inaendelea…….
Nilisoma Government Primary School kwa miaka miwili kisha nikahamia Consolata Primary School, shule ambayo siku hizi inaitwa Shule ya Msingi Chemchem. Shule hii ilikuwa ikimilikiwa na kanisa Katoliki. Sababu za kuhama ni kuwa nilianza kuishi na babu yangu aliyekuwa akiishi Makorongoni, mtaa wa Barabara mbili. Kwenye nyumba ambayo kwa sasa ni kilabu cha pombe maarufu cha Barabara mbili. Na ndiyo ilikuwa nyumba ya babu yangu Mwalimu Raphael Kitime. Aliwahi kunambia kuwa alipopata kiwanja hicho palikuwa na mti mkubwa na alipotaka kuukata alionywa kuwa mti huo hutumiwa na wachawi na hivyo kitu kibaya kingemkuta kama angeukata, lakini yeye anasema aliukata na akajenga nyumba yake na hakuna baya lililomkuta.
Aina ya mti ulikatwa kutengeza uwanja wa Kilabu cha barabara mbili

Wakati huo shule ya Consolata ilikuwa na walimu wengi kati ya ninao wakumbuka waliwemo mwalimu Daudi Luhanga, Mwalimu Kalinga mwalimu wa kiingereza, Mwalimu Filangali mwalimu wa hesabu, Mwalimu Consolata alikuwa mwalimu wa Maarifa, Mwalimu Mkuu akiwa Mwalimu Mwinuka, ni katika wakati huu ndipo naweza kusema dhahiri kuwa hamu ya muziki ilianza kujijenga moyoni mwangu. Hasa kwa sababu ya bendi ya shule. Bendi ya shule ya Consolata, ambayo wakati huo ilikuwa ikiendeshwa na Mwalimu Daudi Luhanga ilikuwa ndio bendi bora kwa shule za primary Iringa mjini wakati huo. Bendi za shule wakati huo zilikuwa ni jambo lililotiliwa maana sana, hasa pale ambapo shule mbalimbali zilikuwa zikikutana, kila shule ilijitahidi kuwa na bendi iliyopiga vizuri na kupambwa vizuri. Bendi ilikuwa na mshika fimbo, ambaye alikuwa na mbwembwe sana, alikuwa akiichezea fimbo yake kwa umahiri kwa kuizungusha kuitupa juu na kuidaka huku akiendelea kutembea kwa step sawa na wenzie, shule yetu ilikuwa na fimbo maalumu iliyotengenezwa nje ya nchi, hilo lilikuwa jambo kubwa sana, lililoifanya bendi hii iwe ngazi tofauti na bendi nyingine, mara nyingi bendi yetu ndio iliongoza paredi ya shule zote katika sikukuu mbalimbali zilizokusanya wanafunzi. Bendi ilikuwa na ngoma kubwa moja, ngoma ndogo mbili na za kati mbili. Ngoma kubwa ilivaliwa begani, wakati ngoma nyingine zilivaliwa kiunoni. Bendi ilikuwa na mtu ambae alikuwa akigonga chuma kilichotengenezwa kwa umbo la pembe tatu, hiki kikiwa na kazi ya kulinda mwendo wa wimbo, pia alikuweko mpiga matasa, matasa ambayo yalitengenezwa kwa kutaka mifuniko ya debe. Wakati huo mafuta ya taa yalikuwa yakifungwa katika madebe na kuuzwa. Mifuniko ilitupwa, lakini debe lilinyooshwa na kupigiliwa juu ya nyumba kama bati. Baada ya hapo kulikuwa na kundi kubwa la wapiga filimbi. Kila siku nilikuwa nikiomba mwalimu Daudi anichague nijiunge kwenye hii bendi lakini sikuchaguliwa. Pale mtaani kwetu watoto tulikuwa tukitengeneza bendi yetu ya makopo na kupita mtaani tukitembea kwa maringo. Siku moja rafiki yetu mmoja ambaye baba yake alikuwa mchungaji, aliweza kupata noti ya shilingi ishirini kwa njia ambazo zina utata. Hii ilikuwa fedha kubwa sana, ngozi ya ng’ombe mzima ilikuwa shilingi tano tu, ile fedha ikatuwezesha kujaribu kutengeneza ndoto yetu ya kuwa na bendi yetu iwe kweli, tuliamua kutengeza bendi yetu. Tulinunua ngozi na kwenda kuiloweka kwenye kisima kilichokuwa jirani, ili baada ya siku saba tuitoe na kuwamba ngoma zetu. Pesa nyingine tukanunua mapipa ya ukubwa mbalimbali na filimbi chache. Siku ya tano tulipata mshituko tulipoenda kukagua ngozi yetu hatukuikuta. Tukaanza msako, haikuchukua muda mrefu tukamjua aliyechukua ngozi yetu, lakini kukawa na uwoga mkubwa kumkabiri alikuwa mtu ambaye watoto wote mtaani tulimuogopa.Kwa siku hizi nyuma tu ya mtaa huu ni stendi kuu ya mabasi Iringa mjini, wakati huo hapo stendi ya sasa palikuwa na makaburi, ambayo yalipakana na makaburi ya Wahindi walipokuwa wakichoma maiti zao. Utotoni hatukujali kuwa palikuwa makaburi muda mwingi tulikuwa tukicheza humo, sema siku tukisikia kuna shughuli ya kuchoma maiti, hatukucheza hapo woga uliingia . 
Mtaani kwetu alikuwepo jamaa mmoja aliyekuwa mkimya sana, siku moja alijaribu kujinyonga kwenye choo nyumbani kwao, katika purukushani kamba ikakatika, akalazwa hospitali muda mrefu. Alipotoka akawa mtu wa ajabu kuliko mwanzo, watoto tulikuwa tukimkimbia kila tukimuona. Lakini huyu bwana akaanzisha shule ya vidudu, akawa na wanafunzi kama kumi hivi. Nae akawa anawafanyisha paredi na kupita nao kwa mstari mtaani, ilikuwa ni kituko lakini mwenye hakuwa anacheka. Tukaambiwa huyo ndiye aliyeiba ile ngozi, na baada ya muda si mrefu shule yake ikawa na ngoma, tuliishia kuwa tunampiga na manati akipita kwenye vichochoro vya mitaa yetu, hatukuweza kumsogelea, wala kumuuliza, wala kutumia watu wengine wamuulize kwani hata sisi ile pesa tulikoipata kungezunga moto mkubwa.

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.