IJUE IRINGA MWANZONI MWA MIAKA YA 60

Mji wa Iringa katika mwanzoni mwa miaka ya 60, haukuwa mkubwa kama ilivyo sasa. Mitaa iliyojulikana sana wakati huo ilikuwa ni Mlandege, Mshindo, Kitanzini, Miyomboni, Makorongoni,  Uhindini, Uzunguni, Mwembetogwa na Ilala. Barabara zote zilikuwa za vumbi, kasoro barabara ya Uhindini na barabara katikati ya mji kuanzia mzunguko wa Samora mpaka idara ya Maji. Uwanja mkubwa wa kufanyia sherehe za sikukuu ulikuwa ni pale ulipo uwanja katikati ya posta na hospitali. Hospitali iliyopo jirani na uwanja ilikuwa inaitwa Grade III, wakati hospitali Grade I ilikuwa ni lile jengo la ghorofa jirani na Magereza. Uwanja huo wa sherehe za sikukuu ulizinduliwa siku ya Uhuru, ukiwa na mnara uliokuwa ukitoka maji juu.

Pia palikuwa na mabembea na mabomba  mbalimbali ya kuchezea watoto. Hapa ndipo ungekuta watoto kutoka mitaa mbalimbali wakikutana kucheza michezo mbalimbali siku za wikiendi. Sikukuu zote kubwa na kiserikali na kidini zilifanyika uwanja huu, kwa kupambwa kwa namna mbalimba kupendezesha uwanja. Barabara kubwa kuingia Iringa kupitia mlima wa Ruaha ilikuwa nyembamba na magari yalikuwa yakipinduka mara kwa mara na kuangukia bondeni, wazo la kupanda miti lilizaliwa miaka ya sabini na wanafunzi wa  shule mbalimbali walifanya kazi ya kupanda miche ya miti inayoonekana leo. Kati ya majengo ya Ibada ambayo tayari yalikuweko miaka hiyo ni Kanisa la Katoliki la Mshindo, Msikiti wa Miyomboni na ule wa Mshindo, Kanisa la Kilutheri  jirani na sokoni, Kanisa lililopo mwembetogwa ambalo lilifahamika kama kanisa la Wanyasa, pia kulikuweko na kanisa la Wasabato la Mlandege, kanisa la katoliki Kihesa, Jamati la Wahindi na nyumba ya Ibada ya Wabaniani zote zikiwa Uhindini.Hakika mtaa wa Uhindini ulikuwa na Wahindi watupu, Mwafrika kuonekana huko ni aidha anatafuta bidhaa au mtumishi wa Wahindi hakukuwa na Mwafrika aliyekuwa akiishi mtaa huo. Kulikuwa na Wahindi maarufu kama Ndumule, huyu aliitwa hivi maana alikuwa akikupa bei ya kitu, akiona unasitasita anakuuliza, ‘Ndumule?’ akimaananisha apunguze bei? Hii ilifanya duka lake kuwa limejaa wateja kila siku. Majengo muhimu mengine yalikuwa ni jengo lililokuwa na mashine za kusaga unga
  pale Mlandege, mali ya Sharif Jamal, Wahehe walipaita kwa Salifu Jama, majengo yaliyo jirani na jengo hilo yalikuwa majengo ya serikali yakiwa yanatumika na idara iliyokuwa inaitwa Public Works Department (PWD), idara hii ilikuja kuitwa Comworks na siku hizi imo katika Wizara ya mawasiliano, hawa walihusika na kujenga na kukarabati miundombinu. Eneo lililopo Uwanja wa Samora lilikuwa awali limegawanyika katika sehemu mbili, lile jengo lililo kushoto kwa geti kuu la Uwanja huo lilikuwa ni klabu ya Wahindi na lilipo jukwaa kuu la uwanja huo palikuwa na uwanja wa tennis.  Ulipo uwanja ulikuwa ni uwanja wa shule ya Iringa Middle School. Na palikuwa na shule pale yenye darasa la 5-8, pembeni yake kulikuwa na nyumba za waalimu na pia upande mmoja nyumba ya Mwalimu Mkuu wa shule hiyo. Hakukuwa na nyumba nyingi jirani ya shule iliyokuwa imezungushiwa wigo wa miti ya minyaa, ambao ulifuata ukuta wa sasa wa Uwanja wa Samora. Jengo la maana nyuma jirani ya shule, lilikuwa jengo la Kilabu cha Kijiweni, ambapo ndipo pekee paliporuhusiwa kuuza pombe za kienyeji. Eneo linaloitwa Frelimo  lilikuwa ni pori na nyumba chache za mjengo wa Kienyeji.  Ukivuka mtaa wa Mwembetogwa na Ilala, ndipo ilikuweko shule iliyoitwa St George na St Michael, ilikuwa shule ya wavulana na wasichana lakini asilimia kubwa ya wanafunzi walikuwa Wazungu. Shule hii ilianza mwaka 1959, ilikuwa maalumu kwa ajili ya watoto wa Wazungu waliokuwa wanafanya kazi Tanganyika wakati huo, ilikuja jengwa kuchukua nafasi ya shule ndogo ya Wazungu iliyokuwa Kongwa, na ilijengwa kwa fedha za Wajerumani katika njia moja wapo ya kujisafisha baada ya vitendo vyao vya kuanzisha vita ya pili ya dunia, mara baada ya Uhuru Waafrika 21 na Wahindi 19 walijiunga na shule hii. 
Shule ya St George na ST Michael wakati inajengwa mwaka 1958

Mabweni ya wasichana mwaka 1961

Wanafunzi wa St George and St Michael 1962

St George &St Michael School kuelekea kwenye Bwalo

Katika eneo ambalo linalo angaliana na ofisi za mkoa kulikuwa na majengo yaliyoezekwa vigae, majengo haya yalikuwa mali ya Sisal Labourers Bureau (SILABU). Hapa kilikuwa kituo cha kufikia wafanyakazi waliokuwa wakitoka mikoa mbalimbali tayari kwa kupelekwa kufanya kazi kwenye mashamba ya mkonge Tanga na Morogoro. Lilipo jengo la Ofisi za Mkuu wa Mkoa ulikuwa ni uwanja wa gofu mali ya Iringa Club. Upande wa Kihesa ulikuwa bado sehemu kubwa ni pori, kanisa la katoliki la Kihesa lilianza kutumika mwaka 1963, kukawepo pia na zahanati na kuanza kupafanya pawe sehemu muhimu. Kituo cha FFU, Kihesa ni kati ya sehemu zilizokuwa zikionekana kuwa nje ya mji miaka hiyo, na hata eneo la askari wake kufanya mazoezi ya kulenga shabaha, ambayo wakati huo yalikuwa nje ya mji kwa sasa ni katikati ya shule ya Lugalo na nyumba za mwanzo wa eneo maarufu la  Kihesa.  

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.