REST IN PEACE EMMANUEL LUNDELE MKUSA


SIKU ya tarehe 19 Julai 2017, ndugu na marafiki wa Emmanuel Lundere Mkusa tulipewa taarifa za kuhuzunisha kuwa mwenzetu huyu hatunae tena. Emmanuel amefariki katika hospitali moja mjini Windhoek, Namibia alikokuwa akiishi na familia yake. Nimefahamiana na Emmanuel, tokea mwaka 1963 huko Iringa, wote tukiwa darasa moja katika shule iliyokuwa inaitwa Consolata Primary School. Siku hizi inaitwa Chemchemu Primary School. Yeye alikuwa akiishi na bibi yake, kaka yake Gerald na dada yake Lucy jirani kabisa na shule hiyo, mimi nikiwa naisihi Makorongoni. Katika utoto wetu tulijikuta katika vitimbi mbalimbali vya utoto ikiwemo kwenda kuogelea Ruaha, jambo ambalo lilikuwa likikatazwa sana na wazazi lakini hakika hatukuwasikiliza tulipoamua. Kwa vile wazazi wake walikuwa wakiishi Dar es Salaam, Emmanuel alikuwa akionekana mtu wa hali ya juu pale alipokuwa akirudi kutoka likizo na kuanza kutusimulia hadithi mbalimbali za jiji hilo ambalo wengine tulikuwa tukilisoma tu kwenye vitabu. Kuna wakati baba yake Emmanuel aliwahi kuja na gari aina ya Morris Minor na tulikuwa tukishangaa utajiri wa akina Emmanuel. Wakati wa uasi wa wanajeshi mwaka 1964, nakumbuka tuliona magari mengi madogo yakiwa na wazungu yakiingia  Iringa yakitokea Dar es Salaam, Emmanuel akanambia Dar es Salaam kuna vita, tukawa tunasubiri vita ifike na Iringa tukaanza hata kupanga tutakimbilia mlima gani kujificha.

Mwaka 1965 wazazi wangu wakahamia Mbeya hivyo nami nikahamishiwa kusoma huko. Lakini tulikutana tena na Emmanuel mwaka 1968 wote tulipochaguliwa kujiunga na shule ya sekondari Aga Khan, shule ambayo siku hizi inaitwa Lugalo. Hapa ndipo nilipokuja kujua uwezo wa ubongo wa Emmanuel, hakuna ubishi kuwa ndugu yetu huyu alikuwa 'genius'. Alikuwa mchezaji mzuri wa basketball, alikuwa mahiri kwenye masomo yote. Akiwa form 2 alishiriki mashindano ya hesabu na kuwa mmoja wapo wa watu watatu bora katika nchi zilizoshiriki mpambano huo ambazo kama kumbukumbu yangu haijakosea ni nchi zote za Afrika Mashariki ikiwemo Zambia. Kufikia form 3 tuliingia pamoja katika mchepuo wa 'Science', nilikuwa najitahidi kufuata nyayo zake hata kwenda kulala kwao ili name niweze kusoma na kuwa mzuri kama yeye, haikuwa rahisi hivyo. Emmanuel aliendelea kufanya maajabu na pia akaanza kutunga michezo ya kuigiza, alikuwa na madaftari kadhaa aliyoandika michezo hiyo, na pia yeye mwenyewe kuigiza, michezo ile aliianza kuandika baada kuwa na sinema mfululizo la Dracula ambazo zilionyeshwa pale shuleni, tulifanya maonyesho kadhaa shuleni kwetu na shule ya Iringa Girls na ukumbi wa mkutano wa CCM Iringa . Na ni wakati huu akaongeza jina lake jingine la Lundere, na kuanza kutambulika kwa jina la Emmanuel Lundere Mkusa. Wiki chache zilizopita alipowasiliana na sie wenzie katika kundi la WhatsApp la waliosoma Aga Khan alikumbusha jina lake la utoto la Katuluta.  Hili jina nakumbuka bibi yake alinambia kuwa lilitokana na yeye kushindwa kusema kaptura wakati akiwa mdogo. Na akaitwa Emmanuel Katuluta kwa wengi tuliokuwa karibu nae, na hakika tumezeeka lakini jina hilo hata mwenyewe alilikubali. Emmanuel Lundere alikuwa bingwa wa hesabu, alikuwa kipenzi cha mwalimu wa Kirusi aliyekuja kutufundisha hesabu tulipokuwa form IV, Miss Uschina, umahiri wake katika hesabu ulinifanya niwe namsindikiza mpaka nyumbani kwa Miss Uschina kwenda kunywa kahawa, na pia kwa uvulana wetu tulikuwa tunafurahi kuwa karibu na mrembo mzungu.

Miezi michache iliyopita nilikutana kwa bahati na dada yake ambaye alinambia Emmanuel ana matatizo anatakiwa kupewa figo nyingine na bahati amepatikana mtu wa kupa figo. Na hapo ndipo tena nikapata mawasiliano na Emmanuel baada ya miaka mingi. Emmanuela alibadilishiwa figo na kuanza kuendelea vizuri kiasi cha kuanza kuishi maisha ya kawaida. Kati ya picha lizotuma kwenye group wiki chache zilizopita alipiga wakati akila maboga na kuonekana na afya nzuri tu. Lakini wiki mbili zilizopita aliaanza kupoteza nguvu na kukohoa sana, jambo ambalo lililosababisha arudi hospitali ambako aligunduliwa kuwa na chembechembe za damu katika mapafu. Kabla ya kuweza kumpatia matibabu Zaidi Emmanuel akafariki. Ngumu kuamini, kwani naona kama juzi tu ndio nilipoiona sabuni ya Cussons kwa mara ya kwanza, na ilikuwa ni Emmanuel aliyekuwa nayo akiwa katoka nayo Dar es Salaam baada ya likizo, nikawa nashangaa nae harufu na povu la sabuni hiyo, hakika ni mambo madogomadogo mengi nayakumbuka. Sitasahau pia tulipoanza kujiona wakubwa na kuanza kujua kupenda wasichana maana yake nini, na hata kuimba nyimbo mbalimbali za kuonyesha mapenzi. Emmanuel alikuwa na record player ambayo ilikuwa na nyimbo kadhaa za Jim Reeves ambazo sasa zinachukua maana nyingine kabisa ntakapokuwa nazisikiliza. Na haswa wimbo Across the Bridge.Across the bridge there is no more sorrow
Across the bridge there is no more pain
The sun will shine across the river
And you will never feel unhappy againMazishi ya Emmanuel yatafanyika Windhoek Namibia, Jumamosi, kwani huko ndiko familia yake iliko.

Mungu amlaze pema Emmanuel Lundere Katuluta Mkusa. 

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.