UNAJUA UHEHE ILIANZAJE? SOMA HAPA

Historia ya Mkwawa  ni historia ambayo imeandikwa sana na inabeba sifa kubwa kwa kabila la wahehe, lakini siku moja baba yangu alinambia kuwa historia hiyo kuna sehemu ina kiza. Haya ni baadhi ya mambo aliyonihadithia kuhusu historia ya Wahehe na Mkwawa.
Ukoo wa Munyigumba ulitawala Ng’uluhe ambako babu yao wa kwanza Mfwimi alifikia akitokea Usagala. Uhehe zamani ilikuwa imegawanyika katika maeneo mengi madogo madogo kama Ng’uluhe, Udongwe, Uhafiwa, Ndevelwa, Luhota, Udzungwa, Lungemba na kadhalika. Na kila eneo lilikuwa na utawala wake, hata hivyo maeneo mengi yalitawaliwa na ndugu wa karibu wa ukoo wa Mwamuyinga kutokana na watemi na watu wenye nasaba bora kuoana wao kwa wao. Na katika mazingira haya Munyigumba aliishi kwa akina Miwhela Mwa Chota aliyekuwa mjomba wake na mtawala wa Luhota.
Huyu Mihwela ndiye aliyeweka jiwe la msingi la kujenga  na kuliimarisha kabila la Wahehe. Mihwela ndiye aliyeanza kukusanya  na kujenga  jeshi la Wahehe, aliwafukuza Wasangu waliokuwa wameingia kwa wingi Uheheni. Kati ya miaka ya 1820-1830 aliwakomesha Waarabu kufanya biashara ya watumwa katika himaya yake, pia aliwakomesha Wamasai kuiba mifugo uheheni.  Mihwela alipokufa  aliacha watoto wawili wa kiume, Muyoveligombo(Muyovela), na Mwengamagoha ambao kwa taratibu ndio walipaswa kutawala Luhota baada ya kifo cha baba yao. Watoto hao wa Miwhela waliamua kumpa ndugu yao Munyigumba sehemu ya mali ya baba yao lakini hawakumpa sehemu ya utawala. Munyigumba aliukataa uamuzi huo, baada ya hapo alitumia kila hila na ujanja na kusababisha watoto hao wa Miwhela kufukuzwa Luhota, na yeye akashika utawala.  Muyigumba aliigawa Uhehe katika maeneo madogo madogo na kila eneo akalipa kiongozi aliyeitwa Mzagila. Hili alilifanya mwaka 1855, mwaka aliozaliwa Mkwawa.
Mwaka 1878, Wangoni waliishambulia Uhehe kwa nguvu, na Munyigumba kulazimika kukimbia na kujificha kwenye mapango ya mlima Nyamulenge. Wangoni walimfuata hukohuko na kuuzunguka mlima huo. Mwanae Mkwawa, ambaye hakika alikuwa bado kijana mdogo alikusanya vikosi vingine vya askari na kuwafuata Wangoni na kuwashambulia kwa nyuma na kuweza kumuokoa baba yake, kisha kuwafukuza Wangoni mpaka kwenye mpaka wa Ubena na Ungoni. Hapo ndipo baba yake alipompa jina la Mkwavinyika.
Katika moja ya vita baina ya Wahehe na Wasangu, Munyigumba alimteka mtu mmoja aliyeitwa Mwamubambe, huyu alikuwa bonge la mtu wa miraba minne, Munyigumba alimpenda mtu huyo na kumuozesha binti yake. Haikuchukua muda mrefu Mwamubambe alianza kutamani kutawala, hivyo akaanza kupanga mipango ya kumpindua Mkwawa,na alifanya mbinu ikalazimika Mkwava  kukimbilia huko jirani na Mpwapwa  sehemu iliitwa Nondova –Wotaponzi, ambako walikuweko wajomba  zake Muyoveligombo(Muyovela) na Mwengamagoha, ambao walikuwa huko toka walipofanyiwa njama na Munyigumba na kutimuliwa Luhota. Huyo Muyovela sasa  nae alikuwa amepata watoto  wawili Mbogamasoli na Msatima. Akiwa hapa Mkwawa  akakusanya jeshi na kurudi Uheheni kufanya vita na Mwamubambe.  Vita kali ilipigwa eneo ambalo sasa linaitwa Lundamatwe (Rundo la Vichwa), kutokana na watu wengi kufa hapo, Mkwavinyika alishinda na kumuua Mwamubambe na kuendelea kutawala Uhehe bila upinzani. Mwaka 1880, Wangoni walishambulia tena Uhehe, safari hii Mkwawa aliwapiga na kuwafukuza mpaka mto Ruhuhu.
Katika vita zake Mkwawa hakuwauza mateka wake kama ilivyokuwa anafanya baba yake, bali aliwafanya watumwa ( Vanyawingi) wa viongozi mbalimbali au watu waliokuwa wa uzao wenye hadhi Uheheni. Kufikia mwaka 1891 jina la Mkwawa lilikuwa maarufu kutokana na kuwa tishio toka Ungoni, Usangu, Ukimbu, Ugogo,Umasai, Unyamwezi, Ulugulu na hata kwa Waswahili wa pwani na Waarabu. Wajerumani  pia walipata taarifa za Mkwaw na waliona kuna umuhimu kudhibiti, ili asije akawafundisha na wengine kupinga utawala wao. Wajerumani walituma kikosi chini ya Mjerumani Von Zelewysk aliyeitwa pia Nyundo. Mkwawa liweza kuwapiga katika vita iliyokuwa ya upande mmoja iliyofanyika Lugalo, Zelewysk alifia hapo na kaburi lake lipo hapo mpaka leo.
kIKOSI CHA wAJERUMANI KIKIELEKEA VITANI

kABURI LA ZELEWYSKY-NYUNDO 
Mubogamasoli na nduguye Msatima walitoka kwao Nondwa (Nondova), na kuja Uheheni kujiunga katika vita. Baada ya hapo Mkwawa akawapa ndugu zake hawa vyeo vya Uzagila. Mbogamasoli akaanza fitna kuhusiana na Mkwawa, utakumbuka kuwa baba zao Muyoveligombo na Mwengamagoha  walifukuzwa Luhota kwa njama za baba yake Mkwawa, Munyigumba. Mkwawa alipogundua kuhusu hizi chokochoko aliamuru Mbogamasoli auawe. Mdogo wake Msatima akakimbilia Kilimatinde.
 Wakati huo Mkwawa alikuwa ameanza kujenga ngome (Lipuli), pale Kalenga(Kwilenga). Ngome hiyo ilijengwa kuzunguka Ikulu (Ivaha au Kwivaha) yake, kwa mzunguko wa kilomita 13. Jina lingine la Lipuli ilikuwa Lilinga au Ilinga.

Msatima alipofika Kilimatinde alikamatwa na Wajerumani na kuhojiwa sana kuhusu Mkwawa na ngome yake, alieleza mengi na ndiyo yalisaidia sana Wajerumani kumshinda Mkwawa kirahisi Wajerumani waliporudi mara ya pili. Mwezi Oktoba 1894, Wajerumani walishambulia ngome ya Mkwawa, safari hii waliongozwa na Mjerumani Von Scheele. Mkwawa alifaulu kukimbia na kuendelea kupigana vita ya msituni kwa miaka mitatu. Hatimae alipoona yu karibu kukamatwa aliona ni heri ajiue na hivyo akajipiga risasi kichwani kule Mlambalasi.

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.